UNICEF yaomba dola za kimarekani bilioni 1.4 kusaidia watoto milioni 45 wanaokabiliwa na hatari za kiafya barani Afrika
2023-12-19 13:50:08| cri

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limeomba dola za kimarekani bilioni 1.4 zitakazosaidia kukwepa mgogoro wa kibinadamu katika eneo la mashariki na kusini mwa Afrika, ambako watoto milioni 45 wako katika hatari ya kukabiliwa na utapiamlo, afya mbaya, kuwa wakimbizi wa ndani na kukosa masomo.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Etleva Kadilli amesema katika taarifa iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya, kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto ni ishara ya wazi kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa kukabiliana na vyanzo vya mgogoro huo na kuwezesha suluhisho endelevu ili kusaidia watoto kukabiliana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa UNICEF, mahitaji yanaongezeka kutokana na makadirio yanayoonyesha uwezekano wa athari kubwa za El Nino kama mafuriko, ambazo zitaendelea mpaka mwanzoni mwa mwaka ujao, na ukame unaotabiriwa kuendelea kwa kipindi chote cha mwaka ujao.