Jeshi la Sudan lathibitisha kuondoka kutoka Wad Madani
2023-12-20 09:04:30| CRI

Jeshi la Sudan (SAF) limethibitisha kuondoa vikosi vyake mjini Wad Madani, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo, baada ya mji huo kuripotiwa kukaliwa na kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Msemaji wa jeshi la Sudan ametoa taarifa ikisema uchunguzi unafanywa kuhusu sababu na hali zilizosababisha kuondoka kwa jeshi hilo, na matokeo yatatolewa mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Kikosi cha RSF jana kilitwaa makao makuu ya Divisheni ya kwanza ya Jeshi la Ardhi la Sudan na kudhibiti Wad Madani, mji mkuu wa jimbo la kati la Gezira, ulioko umbali wa kilomita 170  kusini mashariki mwa mji wa Khartoum.

Kamanda wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo ametoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii akisema raia wa kawaida katika mji wa Wad Madani na jimbo zima la Gezira watakuwa katika hali ya usalama na amani.