Viwanda bubu chanzo kuzagaa bidhaa bandia
2023-12-21 14:32:01| cri

Ongezeko la viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa mbalimbali nchini Tanzania, limeelezwa kuwa pigo kwa wazalishaji halisi, huku Serikali ikiwataka wafanyabiashara kuungana kukabiliana na changamoto hiyo.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah inakuja baada ya wasilisho la Tume ya Ushindani (FCC) jijini Dar es Salaam iliyoonyesha kuwa bidhaa nyingi bandia ilizokamata zimetoka viwanda bubu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza alisema kutokana na kanuni zinazotumika sasa nchini, si lazima kwa kila mmiliki wa kiwanda kuwa mwanachama wa CTI, hivyo kufanya ufuatiliaji wa viwanda kuwa na changamoto.

“Moja ya changamoto tunayokumbana nazo ni kutokuwa na sera wala kanuni inayomlazimisha mwenye kiwanda kuwa mwanachama wa CTI, kungekuwa na sera au kanuni ya namna hii ingekuwa rahisi sana kufanya ufuatiliaji,” amesema Makanza.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia bidhaa bandia kutoka FCC, Khadija Ngasongwa alisema ni muhimu kwa wadau wa biashara, Serikali, sekta binafsi na CTI kuungana ili kuweza kuwafichua wahusika wa bidhaa bandia nchini humo ili viwanda vinavyotengeneza bidhaa halisi viweze kustawi.