Muda wa upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu DRC waongezwa nchini baada ya malalamiko na matatizo ya ugavi
2023-12-21 08:42:52| CRI

Mkuu wa tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Bw. Denis Kadima, amesema upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utaendelea leo alhamis, kwenye vituo vya kupigia kura ambavyo havikufunguliwa jana.

Kutofunguliwa kwa vituo hivyo kulitokana na ucheleweshaji wa vifaa vya kupigia kura na ripoti za ghasia katika baadhi ya vituo vya kupigia kura. Changamoto ilianza kuonekana baada ya baadhi ya vituo vya kupigia kura kuchelewa kufunguliwa huku watu wakiwa wamejipanga kwenye mistari mirefu wakisubiri.

Wagombea watano wa urais, akiwemo Martin Fayulu na Denis Mukwege, wametaka uchaguzi ufanyike upya na wamekataa kutambua upigaji kura uliofanyika Jumatano.

Mbali na ubovu wa mashine za kupigia kura, vituo kadhaa pia vilikabiliwa na uhaba wa karatasi za kupigia kura na vibanda vya kupigia kura. Baadhi ya wapiga kura waligundua kuwa majina yao hayamo kwenye orodha ya wapiga kura.