Waathirika wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda wapongeza hukumu iliyotolewa na mahakama nchini Ufaransa dhidi ya daktari anayehusishwa na mauaji hayo
2023-12-21 23:22:49| cri

Shirikisho la Waathirika wa Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda (IBUKA) limepongeza hukumu ya kifungo cha miaka 24 iliyotolewa na mahakama ya nchini Ufaransa dhidi ya daktari wa zamani wa nchi hiyo, Sosthene Munyemana, kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini Ufaransa, Mahakama hiyo jana ilimkuta Dr. Munyemana kuwa na hatia ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu, na kuhusika katika njama za kupanga mauaji hayo katika wilaya ya Huye, kusini mwa Rwanda.

Rais wa IBUKA Philbert Gakwenzire amesema, ingawa wanapongeza hukumu hiyo, nchi za Ulaya zinapaswa kutafakari upya kwa nini haki imechelewa kutendeka, kwani hukumu dhidi ya daktari hiyo imetolewa miaka 29 baada ya tukio.