IFC yasaini mpango wa kuongeza nyumba za bei nafuu nchini Kenya
2023-12-21 08:41:35| CRI

Shirika la Benki ya Dunia linalokopesha sekta ya kibinafsi, Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), limesaini mkataba wa uwekezaji wa hisa wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 20.9 na Shirika la kimataifa la ujenzi wa nyumba (IHS) Kenya, ili kuongeza upatikanaji wa nyumba za bei nafuu nchini Kenya.

Mkurugenzi wa kanda ya Afrika ya IFC anayeshughulikia viwanda, biashara ya kilimo na huduma Bw. Henrik Elschner Pedersen, amesema msaada huo utatumika kuanzisha mfuko wa kufadhili miradi ya nyumba za bei nafuu.

Amesema uwekezaji wa hisa utasaidia maendeleo na upatikanaji wa takriban nyumba mpya 5,000 za bei nafuu za kijani nchini Kenya.

Mkurugenzi mkuu wa mahusiano ya mtaji na wawekezaji katika IHS Bw. Peter Mayavi, amesema fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa nyumba katika eneo la jiji la Nairobi na kupanuka hadi kwenye kaunti nyingine kulingana na mahitaji.