Usafirishaji wa shehena kwa reli ya SGR nchini Kenya kwa mwaka 2023 watarajiwa kuimarika
2023-12-22 08:40:47| CRI

Ripoti iliyotolewa jana na Shirika la reli la Kenya KRC, imesema huduma ya usafirishaji kwa reli ya SGR nchini Kenya imerekodi ongezeko la asilimia 8 ya shehena katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, huku matumizi yakitarajiwa kushika kasi mwishoni mwa mwaka.

Reli hiyo iliyojengwa na China ilisafirisha tani milioni 4.91 za mizigo kati ya Nairobi na Mombasa katika kipindi hicho, ikiwa ni ongezeko kutoka tani milioni 4.55 za mizigo katika kipindi kama hicho mwaka jana. Idadi ya abiria waliotumia huduma ya usafiri ya SGR pia iliongezeka katika kipindi hicho kutoka abiria milioni 1.74 hadi milioni 1.95.

Shirika la Maendeleo ya Chai Kenya (KTDA) pia limetoa taarifa ikisema reli hiyo imesafirisha mbolea zaidi ya tani elfu 45 za ujazo kwa wakulima wadogo wadogo wa chai, na kusema usafirishaji wa mbolea kwa reli hiyo kunahakikisha ufanisi, kasi, usalama na kupunguza gharama.