China yaikabidhi Botswana kituo cha hali ya hewa
2023-12-22 08:40:05| CRI

Ubalozi wa China mjini Gaborone, Botswana umekabidhi kituo cha hali ya hewa kwa serikali ya Botswana, kwa lengo la kusaidia kuboresha uwezo wa nchi hiyo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Balozi wa China nchini Botswana Bw. Wang Xuefeng amesema, mfumo wa kupokea na kuchakata data za satelaiti uliotolewa na serikali ya China, utatoa msaada mkubwa kwa Botswana katika ufuatiliaji wa mazingira, uzalishaji wa kilimo na kukabiliana na changamoto za matukio mabaya ya hali ya hewa, ili kuisaidia nchi hiyo kufikia malengo yake ya maendeleo endelevu yaliyo rafiki kwa mazingira.

Katibu mkuu wa Wizara ya Mazingira na Utalii ya Botswana Bibi Grace Muzila, alipokea kituo hicho kwa niaba ya serikali ya Botswana na kuishukuru serikali ya China kwa msaada huo. Amesema ukame wa mara kwa mara unazidisha uhaba wa maji na hivyo kuathiri vibaya afya na tija ya watu. Msaada huo utasaidia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha uwezo wa kulinda maisha na mali za wananchi.