Kipyegon, Kiptum watawazwa kuwa wanariadha bora zaidi barani Afrika
2023-12-22 22:31:00| cri

Wanariadha na makocha wa Kenya wametawala tena kwenye tuzo za Shirikisho la Riadha la Afrika (CAA) kwa 2023, na kunyakua tuzo sita kati ya 11.

Nchi hiyo ilisomba tuzo zote bora kwa Mwanariadha Bora wa Kiume na Kike na Wanariadha Wanaochipukia wa Mwaka wa Kiume na Kike. Mwanariadha anayeshikilia rekodi nyingi za dunia Faith Kipyegon na mwanariadha anayeshika rekodi ya dunia ya mbio za marathon Kelvin Kiptum walitangazwa kuwa wanariadha bora zaidi wa kike na wa kiume barani Afrika.

CAA pia ilimtangaza mshindi wa medali ya fedha duniani wa mita 800 Emmanuel Wanyonyi na mshindi wa medali ya shaba duniani wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi, Faith Cherotich kuwa wanariadha Wanaochipukia wa kiume na wa kike.

Kocha wa Kipyegon, Patrick Sang, alitangazwa kuwa Kocha Bora wa Mwaka 2023, huku kocha wa Wanyonyi, bingwa wa Dunia wa mita 800 mwaka 2007 Janeth Jepkosgei, akitangazwa kuwa Kocha Bora wa Mwaka wa Afrika wa 2023.

Kipyegon aliwashinda wanariadha wa Ethiopia, anayeshikilia rekodi ya dunia ya marathon Tigist Assefa na bingwa wa mita 10,000 duniani Gudaf Tsegay ambao wamechukua nafasi za pili na tatu, mtawalia.