Serikali ya Uganda yaanza ufuatiliaji baada ya spishi mpya za mbu kuvamia Kenya
2023-12-23 22:30:23| cri

Meneja wa mpango wa kudhibiti malaria katika Wizara ya Afya ya Uganda, Dkt Jimmy Opigo, amesema wameanza kufanya mchakato wa ufuatiliaji kufuatia tangazo la Kenya kwamba aina mpya ya mbu imevamia katika nchi yao.

“Huyu ni mbu ambaye awali alikuwa Asia, ni mbu wa mijini mwenye fujo. Hivi karibuni amegunduliwa katika Pembe ya Afrika, na Kenya imetangaza. Hivyo sasa tumeanza ufuatiliaji wa suala hilo,” alisema.

Mbu huyo anajulikana kwa jina la kisayansi Anopheles Stephensi lakini kama mbu wengine, kulala ndani ya vyandarua kunaweza kumkinga mtu dhidi ya kuumwa na mbu.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya na ripoti za utafiti, malaria huua Waganda 16 kila siku na kusababisha hasara ya kiuchumi ya dola milioni 500 kwa mwaka (Sh trilioni 1.76) kutokana na gharama za matibabu na muda wa kazi uliopotea.