Watu wanane wafariki na wengine sita kujeruhiwa katika ajali ya basi lililogongana na lori magharibi mwa Tanzania
2023-12-25 09:13:33| CRI

Takriban watu wanane wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya basi dogo maarufu kama mchomoko kugongana uso kwa uso na lori katika mkoa wa Kigoma magharibi mwa Tanzania siku ya Jumapili.

Akiongea na wanahabari katika manispaa ya Kigoma Ujiji, kamanda wa polisi wa mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu, amesema kuwa ajali hiyo ilitokea Jumamosi saa 11 jioni katika kijiji cha Kilemba wilayani Kibondo baada ya dereva wa basi dogo lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kushindwa kulidhibiti basi hilo kwenye kona kali kando ya barabara kuu kati ya Kibondo na Kakonko.

Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, alituma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na kuwatakia majeruhi kupona haraka. Aidha amewataka madereva wa magari kuwa waangalifu hasa katika kipindi hiki cha sikukuu ili kuepuka ajali za barabarani zinazogharimu maisha ya watu wasio na hatia na upotevu wa mali.