UM washirikiana na Tanzania kukabiliana na athari za mafuriko na maporomoko ya udongo
2023-12-25 09:10:38| CRI

Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na serikali ya Tanzania katika kukabiliana na athari za majanga mabaya ya maporomoko ya udongo na mafuriko yaliyotokea tarehe 3 Desemba na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 89 na wengine 5,600 kukosa makazi katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa Jumamosi na Umoja wa Mataifa, ambayo imeendelea kusema kuwa juhudi zinazozingatiwa zaidi kwa pamoja ni kukinga mlipuko wa magonjwa baada ya majanga hayo, kwa kutilia maanani usafi wa maji, mazingira na mahitaji binafsi ya afya haswa katika maeneo waliyotengewa waathirika waliokosa makazi. Na sasa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) yanafanya juhudi za kurejesha usambazaji wa maji safi na kuhimiza watu kuwa na tabia za kujali afya na usafi katika maeneo yaliyoathiriwa, ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa mbalimbali vya msingi vya kukinga magonjwa kwa waathirika.