DR Congo yasubiri matokeo ya awali huku kukiwa na mvutano
2023-12-25 09:14:55| CRI

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuripotiwa kwa matukio ya ukiukwaji wa taratibu katika uchaguzi mkuu uliofanyika Disemba 20.

Wakati nchi hiyo ikisubiri kutangazwa kwa matokeo ya awali huku kukishuhudiwa mvutano, Moise Katumbi, mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani katika kinyang'anyiro cha urais, alisema Jumamosi kwamba uchaguzi wa Disemba 20 unapaswa "kubatilishwa" kwa sababu ya "uwizi mkubwa wa kura".

Wapiga kura milioni 44 nchini DRC walipiga kura Jumatano wiki iliyopita kumchagua rais mpya, wabunge wa Bunge la Taifa na Mabunge ya Majimbo, pamoja na madiwani wa manispaa, huku kukiwa na ucheleweshaji wa kupeleka vifaa vya kupigia kura na kuripoti ghasia za hapa na pale katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI), iliongeza muda wa kupiga kura hadi Desemba 21, ikikiri kwamba baadhi ya vituo vilishindwa kufunguliwa kutokana na matatizo ya vifaa ambayo yalisababisha ucheleweshaji mkubwa wa upigaji kura nchini kote.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, upigaji kura uliendelea Jumapili katika baadhi ya maeneo ya nchi ambayo vituo vya kupigia kura vilikumbwa na ucheleweshaji mkubwa wa vifaa vya kupigia kura.