Waasi wa Houthi wa Yemen wawaonya tena wanajeshi wa Marekani katika Bahari ya Shamu
2023-12-25 09:12:36| CRI

Waasi wa Houthi wa Yemen kupitia msemaji wao Mohammed Abdulsalam, wametoa taarifa iliyopeperushwa kwenye kituo cha televisheni cha al-Masirah cha kundi hilo, wakirudia tena onyo lao kwa vikosi vya Marekani na washirika wao, na kuwataka kuondoka haraka kwenye Bahari ya Shamu kabla haijawa "uwanja unaowaka moto."

Onyo hilo limekuja huku Marekani ikiwashutumu waasi wa Houthi kwa kushambulia meli ya mafuta ghafi ya MV Saibaba, yenye bendera ya India na kumilikiwa na Gabon, kwa kutumia droni, jambo ambalo Abdulsalam alikanusha kwa kudai kuwa wanajeshi wa majini wa Marekani ndiyo walihusika na shambulio hilo la makombora kusini mwa Bahari ya Shamu.

Abdulsalam alifafanua zaidi kuwa wakati ndege ya jeshi lao la wanamaji ikifanya kazi ya upelelezi katika Bahari ya Shamu, meli ya kivita ya Marekani ilifyatua risasi mfululizo kwa kutumia silaha nyingi, akiongeza kuwa moja ya makombora lililipuka karibu na meli ya MV Saibaba, ambayo ilikuwa ikitoka bandari za Russia na kuelekea kusini.

Msemaji huyo alishutumu uvamizi wa kijeshi dhidi ya wa Bahari ya Shamu unaofanywa na Marekani na washirika wake, akisema ni tishio kwa usafiri wa meli baharini na kuwataka kuondoka.