Ifikapo Jumatatu ya tarehe Mosi Januari panapomajaaliwa tutakuwa tayari tumeshaukaribisha mwaka mpya wa 2024. Kawaida unapoanza mwaka kila mtu anakaa na kutafakari ni malengo yepi aliyoyatimiza na yepi yanayohitaji kutiliwa nguvu zaidi ili kuyamalizia. Binadamu hawezi kwenda mbele tu bila kuwa na malengo yoyote, kuna wale wanaotarajia katika mwaka mpya ujao kufunga ndoa, kuanzisha biashara, kujenga nyumba, kutia nia ya kujitahidi zaidi kazini ili kuongezewa mshahara au kupandishwa cheo n.k.
Kuna wanawake wanaotoka nchi mbalimbali ambao kwa hivi sasa wapo hapa nchini China. Wanawake hawa miongoni mwao ni wale wanaotoka Tanzania, na hapa leo tutawasikia wakijieleza wamejipanga vipi katika mwaka 2024, lakini pia tutawaelezea historia fupi tu ya wachina kuanza kutumia mwaka mpya wa Gregori hapa nchini China, maarufu kama Yuan Dan.