Rais Xi Jinping ahutubia Mkutano wa CPC wa Maadhimisho ya Miaka 130 Tangu Kuzaliwa kwa Mao Zedong
2023-12-26 21:47:25| CRI

Kamati kuu ya Chama cha Kikomunisiti cha China (CPC) leo tarehe 26 imefanya mkutano wa kuadhimisha miaka 130 tangu kuzaliwa kwa hayati Mao Zedong katika Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing. Rais Xi Jinping, ambaye pia ni katibu mkuu wa kamati kuu ya CPC ametoa hotuba kwenye mkutano huo akisisitiza kwamba kazi kubwa ya kitaifa iliyoanzishwa na hayati Mao Zedong inatakiwa kusukumwa mbele ambapo mambo ya ustawi wa taifa na ujenzi wa nchi yenye nguvu unapaswa kuhimizwa kupitia ujenzi wa mambo ya kisasa wenye umaalum wa China.

Rais Xi amesema kuwa hayati Mao Zedong, ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa viongozi wa kizazi cha kwanza wa Chama cha Kikomunisiti cha China, ndiye mtu mashuhuri aliyewaongoza wananchi wa China kubadilisha hatma yao na sura ya nchi kwa kina na alipigania kwa maisha yake yote kwa ajili ya kuleta ustawi wa taifa na furaha ya wananchi wa China. Njia bora zaidi ya kumkumbuka hayati Mao ni kuendelea kusukuma mbele kazi hiyo iliyoanzishwa naye.

Rais Xi amesema kuwa kukuza kikamilifu ujenzi wa nchi yenye nguvu na ufufuaji wa taifa kupitia ujenzi wa mambo ya kisasa wenye umaalumu wa China ni kazi kuu ya Chama kizima na wananchi wote wa China katika zama mpya, ambayo ni mambo yanayotarajiwa kutimizwa na hayati Mao Zedong na wanamapinduzi wenzake, na pia ni jukumu zito kwa wanachama wa CPC. Amesisitiza kwamba nia na dhamira ya awali haipaswi kusahaulika na ujenzi wa mambo ya kisasa wenye umaalumu wa China unahitaji kuendelea kuhimizwa.