Serikali ya DRC yakataza maandamano yaliyopangwa kufanyika mjini Kinshasa
2023-12-27 10:08:55| cri

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Peter Kazadi amesema, serikali ya nchi hiyo imepinga kufanyika kwa maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa, yaliyopangwa kufanyika hii leo.

Wiki iliyopita, wagombea watano wa nafasi ya urais walitangaza kuanza maandamano makubwa mjini Kinshasa hii leo ili kupinga udanganyifu katika mchakato wa uchaguzi wa Rais, magavana, wabunge na madiwani uliofanyika tarehe 20 mwezi huu.

Serikali ya DRC imetumia jeshi na polisi ili kudumisha amani na usalama nchini humo, na kuwataka wananchi wake wawe na utulivu na kuendelea kufuatilia matokeo ya uchaguzi huo.