Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning ametangaza uamuzi wa China wa kujibu vikwazo vilivyotolewa na Marekani dhidi ya kampuni moja ya taarifa ya ujasusi ya Marekani Kharon na watu wawili wakiwemo mkurugenzi wa uchunguzi wa kampuni hiyo, Edmund Xu, na mtafiti wa zamani wa Kituo cha Mafunzo ya Juu ya Ulinzi Nicole Morgret, na kuitaka Marekani kuacha kuichafua China.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, hivi karibuni Marekani ilitoa ripoti ya kila mwaka ya haki za binadamu kuhusiana na Xinjiang na kuwawekea vikwazo maafisa wawili wa China na makampuni matatu. Akijibu swali husika kwa waandishi wa habari, Mao Ning alisema hatua hiyo iliyofanya ili kuidhalilisha China na kudhuru haki na maslahi halali ya maafisa na makampuni husika ya China, ni uingiliaji mkubwa wa mambo ya ndani ya China na inakiuka sheria za kimataifa na kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa, hivyo China itachukua hatua madhubuti.
Amesema kwa kutoa ripoti hiyo, Marekani kwa mara nyingine tena ilieneza hadithi za uwongo juu ya Xinjiang na kuwawekea vikwazo kinyume cha sheria maafisa wa China na makampuni kwa kile kinachotajwa kuwa ni masuala ya haki za binadamu. Amesisitiza kuwa China inapinga na kulaani vikali hatua hiyo na kuchukua hatua kubwa dhidi ya Marekani kuhusu hili.