Mkutano kati ya viongozi wa jeshi la Sudan na vikosi vya msaada wa haraka waahirishwa
2023-12-28 09:13:44| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Jumatano ilitangaza kuahirisha mkutano kati ya viongozi wa Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ambao ulipangwa kufanyika Alhamisi nchini Djibouti.

Kwenye taarifa yake wizara hiyo ilisema kwamba iliarifiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Djibouti, nchi mwenyekiti wa sasa wa Mamlaka ya Maendeleo kati ya serikali (IGAD), kwamba Kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo hakuweza kuhudhuria mkutano wake na mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan kutokana na sababu za kiufundi. Taarifa imeongeza kuwa kutakuwa na uratibu tena wa kufanya mkutano Januari mwakani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan pia ilieleza masikitiko yake juu ya ucheleweshaji wa RSF na kutokuwa tayari kukomesha uharibifu nchini Sudan na kuwadhuru watu.