Jeshi la Uganda lasema limemuua kiongozi wa waasi wa ADF kwenye mashambulizi ya hivi karibuni
2023-12-28 09:11:57| CRI

Jeshi la Uganda limesema limemuua kiongozi mkuu wa kundi la waasi la ADF waliohusika na mashambulizi ya hivi karibuni katika wilaya ya magharibi ya Kamwenge.

Katika taarifa yake msemaji wa jeshi la Uganda, Kanali Deo Akiiki, alimtaja kiongozi huyo wa tawi kuwa ni Musa Kamusi, akisema mbali na kumuua kiongozi huyo aliyekuwa akiwahangaisha raia huko Kamwenge, pia walipata bunduki moja ya PK na nyingine ya AK-47 iliyokuwa na risasi kadhaa.

Haya yanajiri siku moja baada ya waasi wa ADF kuwashambulia na kuwaua raia watatu wakiwemo watoto wawili huko Kamwenge. Wiki iliyopita, waasi hao hao waliwaua watu 10 katika wilaya moja. Jeshi limeanza mchakato wa kuajiri askari wa vitengo vya ulinzi vya ndani ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.