Rais Xi Jinping wa China atoa salamu za mwaka mpya wa 2024
2023-12-31 20:59:39| cri

Katika mkesha wa mwaka mpya, rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba ya salamu za mwaka mpya wa 2024 kupitia Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) na mtandao wa Internet. Ifuatayo ni hotuba hiyo:

Hamjambo!

Ukali wa baridi umeanza kupungua na mwaka mpya kukaribia. Wakati mwaka 2024 umewadia, mimi nikiwa hapa Beijing napenda kuwapa salamu za mwaka mpya.

Mwaka 2023, tulikuwa tukiendelea kuchapa kazi na kusonga mbele kwa ushupavu. Tukapata maendeleo zaidi na kuonja utamu wa mafanikio tukikabiliana na changamoto nyingi. Sote tutaukumbuka mwaka 2023 ambao ni mwaka mgumu, lakini pia mioyoni mwetu kumejaa matumaini kwa mwaka mpya wa 2024.

Mwaka 2023 tumepiga hatua kwa madhubuti. Kazi ya kukinga na kuzuia maambukizi ya COVID-19 imepata mafanikio na kuingia katika kipindi cha kawaida. Uchumi wa China uliendelea kufufuka na kuzidi kukua kwa ubora wa hali ya juu. Tumezidi kukamilisha mfumo wa kisasa wa viwanda, na viwanda vingi vya hali ya juu vimeibuka na kuwa nguzo mpya ya uchumi wa China, viwanda hivyo vinatumia teknolojia ya kisasa na kutochafua mazingira. Mwaka 2023, tulipata mavuno makubwa kwa mwaka 20 mfululizo, na ujenzi wa vijiji vyenye mazingira mazuri ukapata maendeleo zaidi, na maeneo ya vijijini yaliendelea kustawi. Eneo la Kaskazini Mashariki ambalo ni eneo la viwanda kongwe limeanza kufufuka, ujenzi wa mji mpya wa Xiong’an unaendelea vizuri, eneo la uchumi la Mto Changjiang limeonesha nguvu kubwa ya kuongoza ukuaji wa uchumi, na uhai mkubwa wa kiuchumi wa eneo la Guangdong-HongKong-Macao umeanza kuonekana.

Mwaka 2023 tumepiga hatua kwa mafanikio halisi. Baada ya jitihada kubwa za miaka mingi, nguvu ya China katika uvumbuzi na uhai wake wa maendeleo zimeanza kuzaa matunda. Ndege kubwa aina ya C919 iliyosanifiwa na kutengenezwa na China imeanza kubeba abiria, meli kubwa ya posta iliyotengenezwa na China imepita kwa mafanikio kwenye safari ya majaribio, vyombo vya safari za anga ya juu vya Shenzhou vinapeleka wanaanga wetu kwenye kituo cha anga ya juu bila kusita, na chombo cha Fendouzhe kilitafiti bahari hadi kwenye kina zaidi. Bidhaa za China zinavutia wateja wengi sana, huku simu za mkononi za aina mpya hata zinauzwa mara baada ya kupelekwa sokoni, na magari yanayotumia nishati mpya, betri za lithium, bidhaa za nishati ya jua Photovoltaic ni bidhaa mpya za China zinazopata wateja wengi kwenye soko la kimataifa. China imesonga mbele kwa moyo wa uchapaji kazi, na kuleta uvumbuzi wa aina mbalimbali.

Mwaka 2023, tumepiga hatua yenye nuru. Michezo ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Duniani ya Chengdu, Michezo ya Asia ya Hangzhou imefanyika kwa mafanikio makubwa, huku wanariadha wakipata matokeo mazuri. Katika siku za mapumziko, watu wengi wamefanya utalii, soko la filamu limestawi, michezo na matamasha vijijini vimevutia, maisha ya kijani yameanza kuwa mtindo mpya wa watu. Utamu wa maisha na ufufukaji wa hali mbalimbali umedhihirisha nia ya watu kwa uzuri na furaha, na pia umeonesha China yenye uhai na ustawi mkubwa.  

Mwaka 2023 tumepiga hatua ya kujiamini. China ni nchi tukufu yenye ustaarabu mkubwa. Katika nchi hii yenye eneo kubwa, mandhari pekee ya jangwani katika sehemu ya Kaskazini Magharibi na manyunyu ya sehemu ya Kusini huwafanya watu wakumbuke na kuvutiwa na historia yake ya maelfu ya miaka. Njia iliyopindapinda ya Mto Huanghe na mawimbi ya kasi ya Mto Changjiang huwafanya watu wawe wachangamfu na kuwa na lengo kubwa. Chimbuko la ustaarabu wa binadamu kwenye miji ya Liangzhu na Erlitou, maandishi kwenye mifupa ya kobe ya Yinxu, mabaki ya utamaduni ya Sanxingdui, urithi wa ustaarabu wa China kwenye Maktaba ya Kitaifa ya Vitabu Muhimu, na kadhalika, hizi historia na utamaduni wetu mkubwa, na pia ni msingi wetu wa kujiamini, na chanzo cha nguvu yetu.

China si kama tu inajiendeleza, bali pia inakumbatiana na dunia, na kubeba majukumu kama nchi kubwa. Tumeandaa kwa mafanikio Mkutano wa Kilele wa China na Asia ya Kati, Kongamano la 3 la Kilele la Ushirikiano wa Kimataifa wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na mikutano mingine, ambapo tumewakaribisha wageni wengi nchini China. Pia nimefanya ziara katika nchi kadhaa, na kuhudhuria mikutano mbalimbali ya kimataifa. Nimekutana na marafiki wakubwa na wenzi wapya, ambapo niliwaelezea mapendekezo ya China na tumekuza maoni ya pamoja. Ingawa mabadiliko hutokea duniani, lakini amani na maendeleo siku zote ni kaulimbiu, na ushirikiano na mafanikio ya pamoja siku zote ni vitu visivyokoseka.

Kwenye njia ya kusonga mbele, ni kawaida kuwa na mvua na upepo. Baadhi ya makampuni yamekabiliwa na shinikizo kwenye biashara, baadhi ya watu wamekumbwa na taabu kwenye maisha, baadhi ya maeneo yameshuhudia majanga ya asili kama vile mafuriko, kimbunga na tetemeko la ardhi, mambo ambayo yote nayafuatilia moyoni. Wananchi hawaogopi mvua na upepo, na kusaidiana wakati wa dhiki, wanakabiliana moja kwa moja na changamoto na kuthubutu kushinda magumu, vitendo ambavyo vimenigusa sana. Wakulima wanaolima mazao mashambani, wafanyakazi wanaochapa kazi kwa bidii, wajasiriamali wenye dhamira ya kuendeleza biashara zao, wanajeshi wanaolinda usalama wa taifa, wananchi wote katika sekta mbalimbali wamekuwa wakitoa jasho, na kila mtu wa kawaida ametoa mchango wake usio wa kawaida! Wananchi daima ni tegemeo letu kubwa kabisa katika kushinda magumu na changamoto zote.

Mwaka kesho ni maadhimisho ya miaka 75 tangu Jamhuri ya Watu wa China ilipoanzishwa. Tunatakiwa kusonga mbele kithabiti na ujenzi wa mambo ya kisasa wenye umaalumu wa kichina, kutekeleza kikamilifu dhana mpya ya maendeleo, kuharakisha ujenzi wa muundo mpya wa maendeleo, kuhimiza maendeleo yenye ubora wa hali ya juu, na kuratibu ipasavyo mambo ya maendeleo na usalama. Tunatakiwa kupiga hatua kwenye msingi imara, kuhimiza utulivu kupitia maendeleo, kuanzisha mambo yaliyo kisasa kabla ya kuondoa yaliyopitwa na wakati, kuimarisha na kuendeleza mwelekeo mzuri wa ufufukaji wa uchumi, na kukuza uchumi kwa njia tulivu na kwa mtazamo wa mbali. Tunatakiwa kuimarisha kwa pande zote mageuzi na ufunguaji mlango, kuinua zaidi imani ya maendeleo, kuongeza uhai wa uchumi, na kutumia nguvu kubwa zaidi kuendeleza sekta za elimu, sayansi na teknolojia na kuandaa vijana wenye vipaji. Tunatakiwa kuendelea kuziunga mkono Hong Kong na Macao kuonesha uwezo na nguvu zao, na kudumisha ustawi na utulivu wakati wa kujiunga vizuri zaidi katika maendeleo ya taifa. Umoja wa taifa letu ni ulazima wa kihistoria, ndugu wa Kando Mbili za Mlango Bahari wa Taiwan wanapaswa kushikana mikono kwa moyo mmoja, na kushuhudia kwa pamoja utukufu mkubwa wa Ustawishwaji Mpya wa Taifa.

Lengo letu ni kubwa, pia ni rahisi. Kwa ufupi, ni kuwawezesha watu waishi maisha bora. Malezi na elimu ya watoto, ajira na mafanikio ya vijana, matibabu na matunzo ya wazee, haya ni mambo ya familia, pia ni ya taifa. Ni lazima tufanye juhudi pamoja na kuyafanya vizuri. Siku hizi, kasi ya jamii yetu ni kubwa, watu wote wana pilika nyingi, na kukabiliwa na shinikizo kubwa sana katika kazi na maisha. Tunapaswa kujenga mazingira mazuri na yenye masikilizano, kupanua nafasi jumuishi na yenye uhai ya uvumbuzi, na kujenga mazingira ya maisha yaliyo rahisi na yenye raha mustarehe, ili watu wote wawe na furaha, kuishi maisha ya mazuri, na kutimiza ndoto.

Hivi sasa, kuna baadhi ya maeneo duniani ambayo bado yako katika mapigano na vita. Watu wa China wanafahamu vyema thamani ya amani, na tuko tayari kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa kwa manufaa ya mustakabali wa binadamu na ustawi wa watu, na kuendeleza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja na kujenga dunia bora.

Katika wakati huu, usiku wenye rangi za kung’ara umeingia na taa zimewashwa katika kila familia. Hebu tutakie pamoja nchi yetu kuwa na ustawi na nguvu, dunia iwe na amani na tulivu! Nawatakia kila la heri na afya njema katika misimu yote!

Asanteni!