Tetemeko kubwa la ardhi latokea nchini Japan na kusababisha vifo na majeruhi ya watu wengi
2024-01-02 08:34:00| CRI

Tetemeko kubwa la ardhi limetokea jana katikati ya Japan na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa, kubomoka kwa nyumba, kukatika kwa umeme na vurugu katika mfumo wa usafiri.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ya nchini humo, matetemeko kadhaa, likiwemo tetemeko kubwa la 7.6 katika kipimo cha Richter lilitokea jana jioni kwa saa za huko katika Peninsula ya Noto, wilaya ya Ishikawa.

Vyombo vya habari vya huko vimesema, baada ya matetemeko hayo, nyumba zilibomoka na barabara kuharibika, na pia moto mkubwa ulitokea katika Wilaya ya Ishikawa na maeneo ya jirani.

Matetemeko hayo pia yalisababisha kutolewa kwa tahadhari ya Tsunami katika pwani ya Bahari ya Japan, na watu wanaoishi katika maeneo ilipotolewa tahadhari, wamehamishwa katika maeneo ya juu zaidi na maeneo mengine kwa ajili ya usalama wao.