UM wazindua mpango wa kuboresha huduma za umma kusini magharibi mwa Somalia
2024-01-02 08:31:24| CRI

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limeshirikiana na wadau muhimu huko Baidoa, mji mkubwa zaidi wa Jimbo la Kusini Magharibi mwa Somalia, ili kuhimiza ushiriki wa jamii na kuboresha huduma za umma.

UNDP imesema ushirikiano huo na Wizara ya Mipango, Uwekezaji na Maendeleo ya Uchumi na Manispaa ya Baidoa, unalenga kuanzisha jukwaa la kidijitali linalohamasisha wananchi, viongozi, mashirika, na wadau kuchangia maendeleo ya mji huo.

Pia limesema lengo kuu la mpango huo ni kuwawezesha watu wa Baidoa, na kuwafanya wawe wachangiaji muhimu wa ujenzi wa jamii yao.

UNDP imesema mpango huo ni sehemu ya Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Saameynta, unaotekelezwa kwa pamoja na UNDP, Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).