Watu 40 wafariki kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
2024-01-02 23:08:35| cri

Mvua kubwa iliyonyesha wiki iliyopita mjini Bukavu, mkoa wa Kivu Kusini ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kuua takriban watu 40.

Mamlaka za huko zimesema takriban watu 20 walipatikana wakiwa wamekufa huko Bukavu na wengine 20 katika kijiji jirani cha Burhinyi. Mamlaka za mkoa zimesema timu za uokoaji zimetumwa kwenye maeneo yaliyoathirika kutafuta wahanga. Wiki iliyopita, takriban watu 20 walikufa kwenye maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika kijiji cha Kalingi katika Wilaya ya Mwenga, Kivu Kusini.

Mwezi Mei 2023, kwenye eneo la Kalehe la Kivu Kusini, takriban miili 438 ilipatikana katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa, na inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 5,000 hawakupatikana. Mafuriko na maporomoko ya ardhi ni ya kawaida nchini DRC wakati wa msimu wa mvua, ambao huanza Septemba hadi Mei, na mara nyingi huwa na athari mbaya.