Uganda yaishataki Kenya
2024-01-04 09:49:50| cri

Uganda imeishitaki Kenya katika mahakama ya Afrika Mashariki baada ya kile imetaja kuwa sheria kali zinazokinzana na makubaliano ya kibishara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC. Serikali ya Uganda iliwasilisha kesi hiyo ikiishutumu Kenya kwa kuizuia nchi hiyo kutumia bomba la Kenya Pipeline KPC kusafirisha mafuta kutoka bandari ya Mombasa hadi Uganda. 

Mwisho wa mwaka jana Kenya ilibadilisha sera za usafirishaji mafuta na kuizuia Uganda kutumia bomba la KPC kujisafirishia mafuta hatua ambayo iliilazimu Uganda kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa muda huku mazungumzo kati ya nchi hizo mbili yakiendelea kutafuta mwafaka namna usafirishaji wa bidhaa hiyo muhimu utarejelewa. 

Uganda inashikilia kwamba mwezi Aprili mwaka jana Kenya ilikuwa imeridhia ombi lake kuiruhusu kutumia bomba la KPC kusafirisha mafuta kabla ya kuchapisha sheria mpya mwishoni mwa mwaka jana na kuinyima Uganda leseni ya kutumia bomba hilo kwa misingi kuwa Kampala haijatimiza matakwa ya wizara ya kawi ya Kenya.