Milipuko miwili iliyotokea karibu na eneo alilozikwa jenerali aliyeuawa wa Iran Qassem Soleimani imesababisha takriban watu 95 kuuawa na wengine zaidi ya 210 kujeruhiwa siku ya Jumatano,.
Vikiripoti kuhusu mlipuko huo, vyombo vya habari vya nchi hiyo vimesema milipuko hiyo ilitokea wakati watu wengi wamekusanyika kwenye makaburi ya mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran, wakiwa kwenye kumbukizi ya mwaka wa nne tangu kuuawa kwa Soleimani katika shambulizi la ndege zisizo na rubani za Marekani.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, mlipuko wa kwanza ulitokea umbali wa mita 700 kutoka kaburi la Soleimani na wa pili ulikuwa umbali wa kilomita moja. Naibu gavana wa jimbo la Kerman anayeshughulikia masuala ya kisiasa na usalama, Rahman Jalali, alisema milipuko hiyo ilitekelezwa na "magaidi,".
Serikali ya Iran imetangaza Alhamisi kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa.