IGAD yatoa wito wa kutatuliwa kwa amani mvutano kati ya Ethiopia na Somalia
2024-01-04 09:03:07| CRI

Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD), Jumatano ilitoa wito wa kufanywa juhudi za kufikia utatuzi wa amani na utulivu wa hali ya sasa kati ya Ethiopia na Somalia.

Wito huo wa dharura ulitolewa na Katibu mtendaji wa IGAD, Workneh Gebeyehu, katika taarifa iliyotolewa Jumatano kuhusu hali ya hivi karibuni ya uhusiano kati ya Ethiopia na Somalia, ambapo alieleza wasiwasi wake mkubwa juu ya hali hiyo. Matukio mabaya ya hivi karibuni kwenye uhusiano baina ya Ethiopia na Somalia yameonekana baada ya Ethiopia na Somaliland, eneo lililojitangazia uhuru la Somalia, kusaini makubaliano ya kuruhusu Ethiopia kufikia Bahari ya Shamu na badala yake iitambue Somaliland kama taifa huru.

Somalia, ambayo inaiona Somaliland kama sehemu ya ardhi yake, ilielezea makubaliano hayo kuwa hayana nguvu za kisheria na kumwita balozi wake nchini Ethiopia kwa ajili ya kujadiliana kuhusu makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi siku ya Jumatatu. IGAD ilisema kwamba "inafuatilia kwa makini" hali hiyo na kutambua athari zinazoweza kuharibu utulivu wa kikanda.