China yaisaidia Afrika kupunguza nakisi yake ya kibiashara na China
2024-01-04 08:49:51| Cri


Baraza la serikali la China hivi karibuni limetangaza kuwa, China itasamehe ushuru wa asilimia 98 wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi sita za Afrika, zikiwemo Angola, Gambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Madagascar, Mali, na Mauritania, kuanzia Desemba mwaka huu. Hii ni moja ya hatua zinazozisaidia nchi za Afrika kuuza zaidi bidhaa zake nchini China, ili kupunguza nakisi zao za kibiashara na China.

Kutokana na maendeleo ya majukwaa ya ushirikiano ikiwemo Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC, na pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", biashara kati ya China na Afrika imeongezeka kwa haraka na mfululizo katika miaka mingi iliyopita. Takwimu zilizotolewa na Idara kuu ya Forodha ya China zinaonesha kuwa, katika zaidi ya miongo miwili iliyopita, biashara kati ya China na Afrika imeongezeka kwa zaidi ya mara 20, na wastani wa ukuaji wa mwaka ni asilimia 14.5. China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 14 mfululizo. Mwaka 2022, biashara ya bidhaa kati ya pande hizo mbili ilifikia dola bilioni 282 za Kimarekani, ambalo ni ongezeko la asilimia 10.9 ikilinganishwa na mwaka 2021, ambapo mauzo ya bidhaa za China barani Afrika ni dola bilioni 164.49 za Kimarekani, huku mauzo ya bidhaa za Afrika nchini China yalikuwa dola bilioni 117.51 za Kimarekani.

Wakati biashara kati ya China na Afrika inaendelea kukua, kama maeneo mengine mengi duniani, Afrika ina nakisi kubwa ya kibiashara na China. Suala hili linafuatiliwa sana na nchi nyingi za Afrika. Kwa upande wa China, haipendi kudumisha urari mzuri wa kibiashara na Afrika, kwani inaona kuwa kuwepo kwa uwiano kutahimiza maendeleo endelevu ya biashara kati yake na Afrika. Hivyo China imechukua hatua mbalimbali ili kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza mauzo ya bidhaa zake nchini China, ili kupunguza na hata kumaliza nakisi yake ya kibiashara na China.

Kusamehe ushuru wa asilimia 98 ya bidhaa za nchi za Afrika ni moja ya hatua muhimu za kuzisaidia nchi za Afrika kupunguza nakisi ya kibiashara na China. Hadi sasa, China imetoa hadhi hiyo kwa nchi 27 za Afrika. Inakadiriwa kuwa thamani ya bidhaa zinazoagizwa na China kutoka Afrika itaongezeka hadi kufikia dola bilioni 300 za Kimarekni mwaka 2035 kutoka dola bilioni 117 mwaka 2022.

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika. Mwaka 2021, mauzo ya bidhaa za kilimo za Afrika nchini China yaliongezeka kwa asilimia 18.2. China imekuwa nchi ya pili duniani kwa wingi wa oda za bidhaa za kilimo za Afrika. Hadi sasa, zaidi ya aina 360 za bidhaa za kilimo za Afrika zimefanikiwa kuingia kwenye soko la China. Miongoni mwao, ufuta, karanga na mazao mengine ya kilimo yamechukua zaidi ya asilimia 80 ya oda za China kutoka nchi za nje.

Licha ya bidhaa za kilimo, baadhi ya makampuni ya China yameanza kuzalisha bidhaa za kiviwanda barani Afrika. Bidhaa hizo ambazo zamani ziliagizwa kutoka China, sasa zinapatikana papo hapo, licha ya kukidhi mahitaji ya Waafrika, pia zinauzwa nchini China. hali ambayo inasaidia sana kupunguza nakisi ya Afrika ya kibiashara na China.

Aidha, China pia imeanzisha majukwaa mbalimbali ikiwemo Maonesho ya Kimataifa ya Uagizaji wa Bidhaa za Nchi za nje ya China (CIIE), na Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika, ili kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza mauzo ya bidhaa zao nchini China.