EU yatoa msaada wa kibinadamu kwa wahanga wa mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Tanzania
2024-01-05 08:35:15| cri

Umoja wa Ulaya (EU) jana ulitangaza kutoa msaada wa kibinadamu wenye thamani ya dola za Kimarekani 110,000 ili kusaidia watu walioathiriwa na maporomoko ya udongo na mafuriko ya hivi karibuni yaliyosababishwa na mvua kubwa katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara, na maeneo mengine ya Tanzania.

Taarifa ya Ujumbe wa Umoja huo kwa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema, fedha hizo zitatumika kusaidia Chama cha Msalaba Mwekundu cha Tanzania katika kufikisha misaada ya dharura na kuzisaidia kaya 44,000 kujikimu kimaisha katika mikoa iliyoathirika zaidi ya Manyara, Dar es Salaam, Kigoma, Kagera, Geita na Unguja.

Maporomoko makubwa ya udongo na mafuriko yaliyotokea tarehe 3 Desemba katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara yalisababisha watu 89 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 5,600 kukosa makazi.