Mwanaume wa Nigeria, 54, aliyemuoa msichana wa miaka minne ili kumwokoa na kifo aibua kelele
2024-01-08 23:32:33| cri

Ndoa kati ya ‘bibi harusi’ mwenye umri wa miaka minne na mwanaume mwenye umri wa miaka 54 katika jamii yenye utajiri wa mafuta ya Bayelsa nchini Nigeria ni ibada ya kitamaduni ya kuokoa maisha ya mtoto huyo, wazazi wa msichana huyo wamesema.

Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Haki za Mtoto, Dk Abayomi Alabi, aliiambia NMG mjini Abuja Jumapili, kwamba baada ya kusikia kutoka kwa wazazi wa mtoto, mtawala wa kitamaduni wa jamii hiyo na mashirika mengine ya kutetea haki, wameamua kulifumbia macho suala hilo.

“Tulikuwa tayari kumkomboa msichana na unyanyasaji huo, lakini maelezo yalikuja kwa wakati mzuri na kupunguza mvutano ambao uliosababishwa na tukio hilo, "alisema.

Ndoa hiyo, ambayo ilifungwa Disemba 26, 2023 katika jamii ya Akeddei katika Eneo la Serikali ya Mtaa ya Sagbama huko Bayelsa ilielezwa ni kama ibada ya kiroho ya 'kuwafungua' wawili hao, ambao walikuwa wamechumbiana katika 'maisha yao yaliyopita'.

Katika utetezi wao, wote walisisitiza kwamba ndoa ya utotoni inayodaiwa ilikuwa ni mila ya kitamaduni inayoitwa "Koripamo" inayolenga kuokoa maisha ya msichana mdogo.

Walieleza kuwa ilikuwa ni mila ya kitamaduni katika jamii ya Akeddei, ukoo wa Oyakiri, kwamba ikiwa mtoto wa kike ataugua kila mara, mwanamume atahitajika kutoa kiasi kikubwa kama ishara ya zawadi ili kumwokoa msichana mdogo asife.

Walieleza zaidi kuwa kila inapofanyika ibada ya kimila ya 'Koripamo', mwanamume aliyelipa zawadi hiyo hatakiwi kumchukua msichana huyo kuwa mke na mila hiyo pia haiwezi kumzuia msichana kuolewa na mwanamume yeyote amtakaye atakapofikisha umri wa kuolewa.