Uganda itafanya biashara na nchi za nje zinazotuheshimu- Museveni
2024-01-10 14:10:42| cri

Katika kujaribu kuzuia shinikizo la kimataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu, Rais Museveni Jumanne alitaka kuwahakikishia Waganda kwamba kila kitu kilikuwa sawa siku chache baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden kuifuta nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwenye mkataba wa kibiashara wa Sh40 bilioni.

Biden alizifuta Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon na Niger kwenye Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (Agoa) kwa misingi kwamba hazikidhi mahitaji ya kuwa kwenye mkataba wa mauzo ya nje.

Mawasiliano ya Disemba 2023 kutoka ofisi ya mwakilishi wa biashara, yalithibitisha kusitishwa huko ambako sasa kunafanya bidhaa za Uganda kuondolewa upendeleo kwenye soko la Marekani. Katika hotuba yake aliyoitoa Jumanne jioni kwa njia ya televisheni huko nyumbani kwao Rwakitura, magharibi mwa Uganda, Rais Museveni, aliwahakikishia Waganda kwamba vikwazo hivyo vya kibiashara na shinikizo "havina maana yoyote." ” kwa sababu Uganda ni taifa la “waundaji utajiri.”