China yasaidia Zambia kupambana na mlipuko wa kipindupindu
2024-01-12 09:30:48| CRI

China imetangaza hatua za kuisaidia Zambia kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu. Balozi wa China nchini Zambia Bw. Du Xiaohui amezindua hatua tisa za kuisaidia nchi hiyo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia.

Bw. Du ametaja hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa fedha, kupeleka wataalam wa matibabu, kuchangia vifaa vya kujikinga, kutoa vifaa tiba, kujenga zahanati katika mkoa wa Kusini na kuchangia matanki ya maji na vifaa.

Bw. Du pia ameunga mkono mradi wa usambazaji maji unaojengwa na Shirika la Uhandisi wa Ujenzi wa Kiraia la China, unaolenga kusambaza maji safi na salama kwa watu wapatao 750,000 huko Lusaka.

Rais Hichilema ameishukuru China kwa msaada huo katika kipindi hiki kigumu, akisema kuwa msaada huo si kama tu utasaidia kuondoa milipuko ya kipindupindu katika muda mfupi, bali pia utasaidia kutokomeza kabisa ugonjwa huo unaosababishwa na maji.