Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi wamefanya mazungumzo mjini Cairo wakijadili njia za kuimarisha uhusiano wa nchi zao na kusisitiza umuhimu wa kutekeleza usimamishaji vita mara moja katika Ukanda wa Gaza.
Bw. Wang amesema China na Misri zimekuwa zikijenga uaminifu wa kisiasa kati yao, ambao umezaa matunda kutokana na ushirikiano wa kivitendo, zikifanya kazi kama nchi zinazowajibika katika masuala ya kimataifa na kikanda, na kufanya uhusiano wa pande mbili uendelee kwa kasi na kufikia kuimarika zaidi, chini ya viongozi wa nchi hizo mbili.
Bw. Wang pia amempongeza rais Sisi kwa kuchaguliwa tena kwa kura nyingi, akielezea imani yake kwamba Misri itapata mafanikio mapya na makubwa zaidi katika kutafuta maendeleo na ustawi wa taifa. Amesema Misri ni nchi muhimu inayoendelea ya Kiarabu, Kiafrika, na Kiislamu, na kwa mara nyingine ameipongeza Misri kwa kuwa mwanachama mpya wa kundi la BRICS.
Rais Al-Sisi ameipongeza China kwa mafanikio makubwa ya kimaendeleo chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping na kwa nafasi yake inayozidi kuwa muhimu katika masuala ya kimataifa. Amesema China ni nchi kubwa, na hakuna nchi inayoweza kuzuia maendeleo ya China, akisisitiza kwamba Misri daima itafuata kanuni ya kuwepo kwa China Moja na kupinga uingiliaji wowote wa mambo ya ndani ya China.
Akitoa shukurani zake kwa China kwa uungaji mkono wake mkubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Misri, rais Sisi amesema ujenzi wa pamoja wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) unaofanywa na Misri na China umekuwa na matokeo mazuri.
Kuhusu mgogoro kati ya Israel na Palestina unaoendelea katika Ukanda wa Gaza, pande hizo mbili zimekubaliana kwamba usimamishaji vita na kukomesha ghasia lazima kufikiwe haraka iwezekanavyo ili kuuzuia mgogoro huo.