Serikali ya Tanzania yafunga mgodi wa dhahabu ulioporomoka huku idadi ya vifo ikifikia 22
2024-01-15 09:49:59| CRI

Serikali ya Tanzania imefunga shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa dhahabu mkoani Simiyu uliobomoka Jumamosi asubuhi na kusababisha vifo vya wachimbaji 22.

Waziri wa Madini Bw. Anthony Mavunde ametangaza kufungwa kwa mgodi huo, na kutangaza kuwa utaendelea kufungwa hadi wataalamu wa madini watakapofanya tathmini ya kina kabla ya kufunguliwa tena.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Bwana Yahaya Nawanda amesema mgodi huo uliporomoka saa 5 asubuhi, na kuongeza kuwa sababu ya kuporomoka kwake ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo Bibi Edith Swebe, amesema kazi ya uokoaji na utafutaji wa watu walionusurika na miili ya watu lilisitishwa Jumamosi usiku baada ya kuthibitishwa kuwa hakuna mtu ndani ya mgodi huo.