Waziri wa mambo ya nje wa China afanya ziara ya kwanza ya mwaka mpya barani Afrika ikiwa ni desturi iliyodumu kwa miaka 34 mfululizo
2024-01-15 10:41:17| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi amefanya ziara katika nchi za Misri, Tunisia, Togo na Cote d’Ivoire kuanzia Januari 13 hadi 18. Huu ni mwaka wa 34 mfululizo kwa waziri wa mambo ya nje wa China kufanya ziara yake ya kwanza ya mwaka mpya barani Afrika. Mwezi Agosti mwaka jana, mazungumzo kati ya viongozi wa China na Afrika yaliyofanyika huko Johannesburg, Afrika Kusini yalizua mjadala mkubwa, na mwaka huu mkutano wa awamu mpya wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utafanyika China. Katika hali hiyo, ziara hii ya waziri wa mambo ya nje ya China imetoa ishara yenye nguvu ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Nia ya asili ya China ya kushirikiana na nchi za Afrika haibadiliki na haitabadilika. Waziri wa mambo ya nje wa China hufanya ziara yake ya kwanza ya mwaka mpya katika bara la Afrika, desturi ambayo ni pekee katika historia ya mawasiliano ya kimataifa. Desturi hiyo inatokana na mahitaji halisi ya China na Afrika kuimarisha ushirikiano na kutimiza maendeleo kwa pamoja. China imekuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 14 mfululizo. Katika miaka iliyopita, China imejenga reli yenye urefu zaidi ya kilomita elfu kumi, barabara yenye urefu zaidi ya kilomita laki moja, madaraja zaidi ya elfu moja, bandari karibu mia moja pamoja na hospitali na shule nyingi katika nchi za Afrika, matunda hayo ya ushirikiano yamethibitisha uungaji mkono thabiti wa China kwa maendeleo na ustawi wa Afrika. Katika mazungumzo kati ya viongozi wa China na Afrika yaliyofanyika mwaka jana, China ilitangaza kuanzisha Pendekezo la Kuunga mkono Maendeleo ya Viwanda barani Afrika, kutekeleza Mpango wa China Kuisaidia Afrika Kuendeleza Kilimo cha Kisasa na Mpango wa Ushirikiano wa China na Afrika wa Kuandaa Vijana wenye Vipaji, ambao ni pamoja na kuandaa wakuu na walimu 500 wa shule za ufundi stadi, kuandaa vijana elfu kumi wenye uwezo wa lugha ya kichina na ufundi stadi, na kualika maofisa wa serikali na mafundi bingwa kutoka nchi za Afrika kushiriki kwenye semina na mafunzo mbalimbali kila mwaka. Hatua hizo tatu zimegusa sekta zinazohitajika zaidi Afrika katika kuendeleza mambo ya kisasa, ni hatua halisi zinazochukuliwa na China kuunga mkono maendeleo ya Afrika, ambazo zimekaribishwa sana na viongozi wa Afrika walioshiriki kwenye mazungumzo hayo. Ziara hii ya Bw. Wang Yi inalenga kusukuma mbele utekelezaji wa matunda yaliyopatikana kwenye mazungumzo hayo, na kutoa ishara bayana kuwa China daima iko pamoja na nchi za Afrika.

Marafiki wa China katika bara la Afrika wameongezeka zaidi. Nchi nne za Afrika alizotembelea Bw. Wang Yi katika ziara hiyo zote ni wenzi wakubwa wa ushirikiano wa China. Nchini Misri, Eneo la Ushirikiano wa Kiuchumi la TEDA Suez kati ya China na Misri limevutia makampuni zaidi ya 140, ambayo yametoa nafasi za ajira kwa wenyeji zaidi ya 5,000 wa Misri, eneo hilo limekuwa mfano wa watu wa Misri kunufaika na ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Nchini Tunisia, China imejenga hospitali kuu, chuo cha mafunzo ya diplomasia, kituo cha utamaduni na michezo kwa vijana cha Ben Arous, na miradi mbalimbali ya miundombinu ya kiraia ikiwemo ujenzi wa bwawa la mto Mellegue, imeendelea vizuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa mwaka huu, kampuni ya China imepata kandarasi ya kujenga mradi wa daraja la Bizerte. Huko kaskazini mwa Togo, timu ya teknolojia ya kilimo kutoka China imefanikisha majaribio ya upandaji mpunga, na kubadilisha historia ya huko kutoweza kupanda mpunga katika majira ya kiangazi, na mbuga za majaribio zimeongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa. Huko mjini Abidjan nchini Cote d’Ivoire, daraja la Cocody lililojengwa na kampuni ya China limeanza kutumika na kupunguza kidhahiri msongamano wa magari mjini humo, na daraja hilo limekuwa moja ya alama za mji huo. Ziara hiyo ya Bw. Wang Yi itasukuma mbele ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika uzae matunda mengi zaidi, na kunufaisha zaidi watu wa China na Afrika.