Umoja wa Mataifa waeleza matarajio ya kutimiza amani nchini Sudan
2024-01-15 10:43:21| cri

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Ramtane Lamamra ameeleza matarajio yake kuhusu uwezekano wa kutimiza amani na utulivu na kumaliza mapigano nchini Sudan.

Lamamra amesema hayo jana jumapili alipokutana na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Mpito la Sudan na Kamanda wa Jeshi la nchi hiyo, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan katika mji wa Port Sudan.

Taarifa iliyotolewa na Baraza hilo imesema, Lamamra amesema amefanya mazungumzo na maofisa na wawakilishi wa mashirika ya kiraia ya nchini Sudan, na ameahidi kufanya kazi na pande zote zinazohusika ili kutimiza wajibu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro huo.

Kwa upande wake, Jenerali Al-Burhan amemwarifu mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu juhudi za kutafuta suluhisho la amani, akisisitiza ahadi ya serikali ya Sudan ya mageuzi ya kidemokrasia na kipindi cha mpito kitakachomalizika kwa kufanyika kwa uchaguzi mkuu.