Wataalamu wakutana nchini Kenya kuhimiza biashara chini ya AfCFTA
2024-01-16 09:28:41| CRI

Wataalam wanaendelea na mkutano wa siku tatu mjini Nairobi ili kuhimiza biashara chini ya Makubaliano ya Eneo Huria la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Mkutano wa kwanza wa mikakati ya utekelezaji wa AfCFTA uliwakutanisha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, pamoja na maofisa wa serikali kutoka zaidi ya nchi 40 za Afrika ili kupitia upya njia za kufanya biashara huria katika bara hilo.

Mkurugenzi wa kitengo cha ushirikiano wa kikanda na biashara katika Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) Bw. Stephen Karingi, amesema kwenye hotuba yake ya ufunguzi kwamba AfCFTA inashikilia ahadi kwa bara la Afrika kuondokana na kasumba ya ukoloni ya kuwa masoko madogo na yaliyogawanyika na badala yake kuunda soko moja kubwa lenye watu zaidi ya bilioni 1.4.

Bwana Karingi amesema soko moja la bara linatarajiwa kuunda kiwango cha kuvutia uwekezaji mkubwa wa minyororo ya thamani ya kikanda, na ukuaji wa viwanda.