Tanzania yasitisha safari za ndege za shirika la ndege la Kenya kati ya Nairobi na Dar es Salaam
2024-01-16 09:40:21| CRI

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania imetangaza kusimamisha safari zote za abiria za Shirika la Ndege la Kenya kati ya Nairobi na Dar es Salaam, kuanzia Januari 22, mwaka 2024.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema katika taarifa yake kwamba hatua hiyo ni kujibu Kenya hivi karibuni kukataa ombi la Tanzania la kuruhusu shirika lake la ndege la Air Tanzania kufanya safari za mizigo kati ya Nairobi na nchi ya tatu.

Kwenye taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari, TCAA ilitaja kukataa kwa mamlaka ya Kenya kuwa ni ukiukaji wa Kifungu cha 4 cha mkataba wa makubaliano kuhusu Huduma za Ndege uliosainiwa kati ya nchi hizo mbili mwaka wa 2016. Tanzania imefanya juhudi kufuata kanuni za kimataifa za usafiri wa anga na mikataba ya nchi mbili.