China na Togo zinatarajia ushirikiano wa karibu zaidi
2024-01-18 09:54:37| CRI

Rais Faure Gnassingbe wa Togo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi walikutana Jumatano mjini Lome, wakieleza nia ya kukuza uhusiano wa nchi zao na kuendeleza ushirikiano kati ya Afrika na China.

Rais Gnassingbe amesema kutokana na utaratibu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, Togo na nchi nyingine za Afrika zimepata maendeleo katika ujenzi wa miundombinu, na kwamba Afrika imeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wake, kuimarisha usalama na kuleta manufaa kwa watu wa bara hilo. Amesisitiza kuwa mafanikio haya yasingeweza kupatikana bila msaada wa muda mrefu na wa kujitolea wa China.

Amesema Togo inaishukuru China kwa kudumisha haki katika jukwaa la kimataifa, kupinga uingiliaji kati masuala ya ndani ya Afrika, na kuchukua nafasi muhimu katika maendeleo ya amani ya Afrika.

Waziri Wang ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, amesema urafiki kati ya China na Togo, ulioanzishwa na viongozi wa kizazi cha zamani, umekuwa mfano wa kuigwa wa ushirikiano wa Kusini na Kusini.

Amesema China itaimarisha ushirikiano wa mikakati ya maendeleo na Togo na kuisaidia Togo katika kufikia maendeleo endelevu.

Amesema China inaelewa na kuiamini Afrika, akibainisha kuwa maadam Afrika ina umoja na uhuru, inaimarika kupitia umoja, na kutafuta njia ya maendeleo inayoendana na hali ya taifa, itaweza kushinda matatizo na kuunda fursa mpya.