China na Togo zakubaliana kutekeleza ipasavyo matokeo ya ushirikiano kati ya China na Afrika
2024-01-18 09:56:22| CRI

Waziri Mkuu wa Togo Victoire Sidemeho Tomegah Dogbe na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi wamekubaliana kuhimiza utekelezaji wa matokeo ya ushirikiano kati ya China na Afrika.

Akizungumza na Bw. Wang Jumatano mjini Lome, Dogbe aliishukuru China kwa msaada wake kwa maendeleo ya Togo, na kwamba Togo itaendelea kufuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na inaunga mkono China katika kufanikisha umoja wa kitaifa mapema.

Amesema Togo inafurahia mafanikio makubwa ya maendeleo ya China na inatarajia kujifunza kutoka kwa China na kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile kupunguza umaskini, kilimo, maeneo ya viwanda, ili kuunda nafasi nyingi zaidi za ajira na kufikia ukuaji jumuishi na endelevu. Bw. Dogbe ameongeza kuwa Togo inakaribisha uwekezaji zaidi kutoka kwa makampuni ya China.

Dogbe amesema Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) limetoa mchango mkubwa katika kuharakisha maendeleo ya Afrika, na "Miradi Tisa" iliyopendekezwa na Rais Xi Jinping wa China imeinufaisha sana Togo, na kwamba Togo iko tayari kushirikiana na China kujiandaa kwa mkutano ujao wa FOCAC.

Waziri Wang ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, amesema katika kipindi cha nusu karne iliyopita, China na Togo zimesaidiana kithabiti katika masuala yanayohusu maslahi yao makuu na ufuatiliaji mkubwa, na kuzidisha hali ya kuaminiana kisiasa na ushirikiano unaoendelea kunufaisha pande zote mbili. Amesema FOCAC imekuwa jukwaa muhimu la kukuza maendeleo ya Afrika, imekuwa bendera ya mshikamano na ushirikiano kati ya China na Afrika, na imeongoza ipasavyo ushirikiano wa kimataifa na Afrika. Amesisitiza kuwa China itaendelea kuzisaidia nchi za Afrika kutafuta njia za maendeleo zinazoendana na hali zao za taifa.