Nchi zisizofungamana na upande wowote zashinikiza kuwa na sauti zaidi katika masuala ya kimataifa
2024-01-18 10:07:08| CRI

Nchi wanachama wa Harakati ya kutofungamana na upande wowote (NAM) zinazoendelea na mkutano nchini Uganda, zinashikilia msimamo wa kuhakikisha kuwa harakati hiyo yenye wanachama 120 ina sauti zaidi katika masuala ya kimataifa.

Makamu wa Rais wa Uganda Bibi Jessica Alupo, amesema wakati akifungua Mkutano wa Mawaziri wa siku mbili wa harakati hiyo, kuwa Harakati hiyo inakutana wakati mivutano ya siasa za kijiografia inaongezeka. Amesema kutokana na kuwepo kwa matukio kama haya kwenye mikutano ya kimataifa, nchi wanachama zinapaswa kuwa na umoja na kushikamana na kufuata kanuni za msingi za Harakati hiyo, ikiwa ni pamoja na kuheshimu uhuru na ukamilifu wa ardhi ya mataifa yote, kutambua usawa wa rangi zote na usawa wa mataifa yote, makubwa na madogo, na kujiepusha kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine.