Watoto 10 kufanyiwa upasuaji wa moyo Zambia
2024-01-19 23:36:34| cri

Watoto 10 waliozaliwa na matatizo ya moyo wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya upasuaji inayofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Moyo nchini Zambia.

Kambi hiyo ya siku nne inafanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ya nchini Tanzania kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Taifa ya Moyo iliyopo jijini Lusaka, Zambia.

Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Godwin Sharau amesema, katika kambi hiyo wanafanya upasuaji wa kuziba matundu ya moyo, kurekebisha valvu za moyo pamoja na kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake.