Kenya yapata mkopo wa dola milioni 684 kutoka IMF
2024-01-19 09:36:04| CRI

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeidhinisha mkopo wa dola milioni 684.7 za kimarekani ili kuisaidia Kenya kufadhili mipango mbalimbali ya maendeleo wakati ikiwa na changamoto za kiuchumi.

IMF imesema dola milioni 624.5 zitatolewa mara moja chini ya mpango wa Mfuko wa Upanuzi wa Hazina (EFF) na msaada wa kulipa madeni (ECF) huku dola milioni 60.2 zitatolewa chini ya mpango wa uendelevu wa uchumi (RSF).

Taarifa iliyotolewa wiki hii inasema uchumi wa Kenya unaendelea kustahimili hali ngumu hata unaporejea kutoka kwenye janga la COVID-19, na ukame mkali katika miaka miwili iliyopita.

Mkopo huo ambao uliidhinishwa Aprili 2021, unalenga kusaidia mpango wa Kenya wa kushughulikia changamoto ya kulipa madeni, kukabiliana na janga la COVID-19 na majanga ya kimataifa, na kuimarisha utawala na mageuzi ya kiuchumi.