China na Cameroon zaahidi kutafuta mafanikio mapya ya ushirikiano
2024-01-19 09:33:23| CRI

Naibu waziri mkuu wa China Liu Guozhong, aliyeongoza ujumbe wa serikali ya China alitembelea Cameroon Jumatano na Alhamisi. Katika ziara hiyo alikutana na rais na waziri mkuu wa nchi, ambapo pande zote mbili zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Akizungumzia mafanikio ya maendeleo ya Cameroon, Bw. Liu amesema katika miaka 52 ya uhusiano wa kidiplomasia na China, nchi hizo mbili zimekuwa zikitendeana kwa udhati, na zimepata matokeo mazuri katika ushirikiano, na kuendelea kuimarisha uhusiano wa kirafiki. Bw. Liu ameeleza nia ya China ya kuzidisha hali ya kuaminiana ya kisiasa na Cameroon, kuimarisha ushirikiano wa mikakati yao ya maendeleo, kushikilia kanuni za kunufaishana.

Pia amesema China inapenda kushirikiana na Cameroon katika masuala ya kimataifa, kuhimiza ushirikiano wa Kusini na Kusini, kulinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, na kuchangia katika kujenga jumuiya ya ngazi ya juu yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika.

Rais Paul Biya amesema Cameroon inashikilia kwa uthabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na haitabadilisha sera na msimamo wake katika suala hili. Naye waziri mkuu Ngute amesema nchi hizo mbili zina historia ndefu ya urafiki na ushirikiano wa karibu. Ameeleza nia ya Cameroon kuzidisha ushirikiano na China, ili kuleta manufaa zaidi kwa watu wa Cameroon na China na kusukuma mafanikio mapya katika maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo.