Bandari za Mombasa na Dar zaendelea na ushindani huku mizigo ikiendelea kuongezeka
2024-01-23 23:01:44| cri

Kiasi cha mizigo kwenye bandari za Mombasa na Dar es Salaam kinaendelea kuongezeka huku kukiwa na ushindani mkubwa.

Wiki hii bandari ya Dar es salaam ilitangaza kukamilisha mradi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 420 na inapanga kupanua miundombinu yake na kufungua sehemu ya kuhifadhi mizigo inayopelekwa katika nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mbossa, amesema walipanga ujenzi wa magati sita mapya ya Dar na Bagamoyo, kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Utendaji wa sasa wa Bandari ya Dar es Salaam ni wa chini ukilinganishwa na Mombasa, Beira na Durban, na kuwalazimu wasafirishaji wakuu kuikwepa kutokana na gharama na muda wa kusubiri kwa meli kushusha mizigo. Kushusha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam huchukua siku 5, ikilinganishwa na siku 1.25 Mombasa na siku 1.6 Durban.