Waziri Mkuu wa Somalia akutana na wakuu wa usalama kwa lengo la kuboresha usalama nchini humo
2024-01-24 08:31:14| CRI

Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre ameongoza mkutano wa dharura na maofisa wa ngazi ya juu wa usalama nchini humo kwa lengo la kujadili hali ya usalama nchini humo.

Ofisi ya Waziri Mkuu jana imesema, mkutano huo uliofanyika mjini Mogadishu, ulilenga zaidi katika operesheni za kulitokomeza kundi la al-Shabaab ambalo limefanya mashambulio kadhaa ya kigaidi nchini humo, na juhudi za kuboresha ulinzi wa nchi hiyo.

Katika mkutano huo, Barre alisisitiza dhamira ya serikali ya kukabiliana na changamoto za usalama zinazoikabili Somalia.

Mkutano huo umefanyika wakati kuna mvutano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Ethiopia ambao umesababisha rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud kufuta makubaliano yaliyofikiwa kati ya Ethiopia na mkoa wa Somaliland yanayoruhusu Ethiopia kutumia Bahari Nyekundu kufuatia nchi hiyo kuitambua Somaliland kama nchi huru.