Katibu Mkuu wa UM atoa wito wa kuchukua hatua za haraka kupambana na ugaidi barani Afrika
2024-01-25 08:30:14| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza haja ya kukabiliana na ongezeko la ugaidi barani Afrika, akiielezea hali hiyo kuwa ni hatari ya wazi sio tu kwa bara hilo, bali kwa dunia nzima.

Akizungumza katika mkutano wa Mkataba wa Kupambana na Ugaidi Duniani uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New York, Marekani, Guterres amesema katika miaka michache, Afrika imekuwa kituo cha ugaidi duniani, na kwamba katika mazingira hayo, wanawake na watoto wa kike wako hatarini zaidi kufanyiwa unyanyasaji wa kimapenzi na uhalifu wa kijinsia.

Amesema katika maeneo kama Somalia, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kaskazini mwa Msumbiji na kanda ya Sahel, raia wanakabiliwa na mapigano na machafuko, wakiishi maisha magumu yasiyo na matumaini.