Sh42.6 bilioni kurekebisha barabara zilizoharibiwa na mvua Tanzania
2024-01-25 23:00:04| cri

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) ameomba Sh42.6 bilioni kwa ajili ya marekebisho ya barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha Tanzania.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa ameitaka TARURA itumie fedha hizo kuchimba mitaro mirefu inayoelekeza maji katika maeneo stahiki ili kuepusha kukwama shughuli za kijamii kutokana na barabara kujaa maji.

Agizo hilo amelitoa siku chache tangu mvua iliyonyesha ndani ya Jiji la Dar es Salaam Januari 20 na 21, kukwamisha baadhi ya shughuli za kiuchumi baada ya kingo za madaraja kumeguka na barabara nyingine kufungwa kutokana na maji kujaa.

Waziri Mchengerwa amesema hayo wakati wa kikao kazi kilichowashirikisha Tamisemi, Tarura, Makatibu Tawala Wasaidizi (Miundombinu), wakandarasi wazawa, wataalamu washauri na taasisi za kibenki, kilicholenga kuwawezesha wakandarasi hao kuchangamkia fursa za miradi mbalimbali nchini.