Nchi wanachama wa NAM zaipongeza China kwa juhudi zake za kudumisha amani ya dunia
2024-01-25 08:29:35| CRI

Maofisa wa ngazi ya juu kutoka Uganda, Sudan na Bolivia wameipongeza China kwa nafasi yake katika kuboresha usawa katika masuala ya kimataifa.

Wakizungumza na Shirika la Habari la China Xinhua wakati wa mkutano wa 19 wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) uliofanyika nchini Uganda, maofisa hao wamesema China imekuwa ikichukua nafasi muhimu katika ustawi wa kisiasa, kijamii na kiuchumi katika nchi zinazoendelea.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Al-Sadiq amesema, China ni mwenzi muhimu wa Afrika, kwa kuwa nchi hiyo imejikita katika maendeleo ya nchi za Afrika bila ya kuwa na masharti yoyote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Okello Oryem amepongeza nafasi ya China katika mgogoro unaoendelea katika Ukanda wa Gaza, na kusema China daima imekuwa mtetezi wa suluhisho la amani katika migogoro.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Bolivia, Celinda Sosa Lunda ameielezea China kama mwenzi wa maendeleo wa nchi hiyo, na kusema Bolivia inaungana na msimamo wa China katika kutatua mgogoro kati ya Israel na Palestina.