Afrika Mashariki yarekodi ongezeko la mavuno ya mahindi kufuatia mvua za El Nino
2024-01-26 08:30:26| CRI

Kanda ya Afrika Mashariki inatarajia kuwa na mavuno makubwa ya mahindi itakapofika mwezi Septemba mwaka huu baada ya mvua za El Nino kuboresha uzalishaji, hususan katika nchi ambazo zina uhitaji mkubwa wa nafaka.

Hayo yamo kwenye ripoti ya pamoja iliyotolewa jana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na wenzi wake, ambayo imesema kanda hiyo itakuwa na ziada ya tani za ujazo milioni 1.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia 116 kutoka zile za mwaka 2023.

Ripoti hiyo imesema, nchi zenye uzalishaji hafifu, ikiwemo Kenya, Sudan Kusini, Somalia na Rwanda zinatarajia kuagiza mahindi kutoka Uganda, Tanzania, na Ethiopia ili kukabiliana na upungufu huo.

Ripoti hiyo pia imesema, nafaka nyingine ambazo uzalishaji wake umeongezeka katika kanda hiyo kutokana na mvua kubwa za El Nino ni maharage, mchele na mtama.